Ili uweze kufikia malengo yako ya kimasoko katika kutangaza huduma au bidhaa za kampuni yako, kutumia waraghbishi (Influencers) ni njia nzuri. Kufanya masoko kupitia waraghbishi (Influencer Marketing) imekuwa ni mbinu mpya na nzuri kwa makampuni, taasisi na hata mashirika katika miaka ya hivi karibuni.

Mraghbishi (Influencer) ni mtu wa aina gani? Ni mtu ambaye ana ushawishi katika hadhira yake, na kampuni inayotangaza inakusudia kutumia ushawishi wake kuhakikisha kuwa inawafikia watu wengi zaidi na kutimiza malengo yake ya kimawasiliano au ya kibiashara. Kuna aina nyingi za waraghbishi kulingana na mahitaji ya biashara;

 • Waraghnishi wakubwa sana (mega influencers). Hawa ni watu maarufu na wenye ufuasi mwingi mtandaoni  na nje ya mtandao kama wasanii na wanamichezo. Hawa si lazima wawe wanafanya mambo yanayoendana na biashara yako. Huwa na kuanzia wafuasi milioni moja na zaidi
 • Waraghbishi wakubwa (Macro Influencers). Hawa ni waraghbishi ambao mara nyingi ni maarufu zaidi mitandaoni, na hawakutokana na umaarufu wa kisanaa au michezo au siasa. Huwa na wafuasi kuanzia 1,00,000-1,000,000.
 • Waraghbishi wa kati (Micro Influencers). Hawa ni wale ambao wana ufuasi wa wastani, na mara nyingi kama ni wasanii au wanamichezo au hata watengeneza maudhui ya mitandaoni, basi ndiyo wanachipukia. Huwa na wafuasi 1,000-100,000
 • Waraghbishi mawakili (Advocates). Hawa huwa wanakuwa mtandaoni na huzungumzia mema au kutetea kuhusu biashara yako. Mara nyingi huwa na wafuasi wachache
 • Waraghbishi waunganishaji (Referrers). Hawa ni wale wanaoshawishi watu kufanya uchaguzi wa bidhaa zako, na wanaweza kuwa bloggers au wanamtandao wanaofanya mapitio ya bidhaa na huduma (product and service reviews)
 • Waraghbishi watiifu (Loyalists). Hawa ni wateja wa kawaida, mashabiki, na wafuasi wako. Hutengenezwa na biashara yenyewe kupitia mawasiliano chanya ya mara kwa mara, kuwahusisha katika matukio ya biashara, kuwapa ofa nzuri na kuwaunga mkono kila inapowezekana.

Makala hii inaangazia hatua ambazo kampuni, taasisi au biashara yako inaweza kupitia ili kujenga mkakati wa matumizi sahihi na wenye mafanikio ya Influencers;

 1. Tambua na bainisha malengo yako

Hatua ya kwanza ya kufanya masoko kupitia waraghbishi ni kuweka malengo yako kwa kubainisha kwa uwazi kile unachotaka kufanikisha. Unapaswa kuangalia ni vitu gani utapima ili kujua ikiwa umefanikiwa kulingana na malengo uliyoweka. Kwa kufanya hivi, itakusaidia kufahamu unahitaji kufanya nini ili kufikia malengo yako.

Vilevile, unapaswa kutambua hadhira lengwa. Je unamlenga nani katika mpango wako huo wa kutumia waraghbishi? Mara nyingi, hadhira lengwa hutegemeana na aina ya bidhaa au huduma unayokusudia kuitangaza.

Ni kundi gani katika jamii linaweza kuhitaji huduma au bidhaa zako? Ni kitu gani wanapenda, hawapendi na yapi machaguo yao? Ni namna gani unaweza kuitangaza huduma au bidhaa kwa namna ambayo itawafaa mahitaji yao?

Melengo ya kutafuta masoko kupitia kampeni ya waraghbishi  hutofautiana, lakini kampuni na taasisi nyingi hukusudia kufikia malengo yafuatayo;

 • Kutengeneza mahusiano imara na hadhira/wateja
 • Kuongeza mauzo na faida
 • Kuongeza ushawishi wa kampuni, na
 • Kuongeza kufahamika kwa kampuni

2.Tafuta Waraghbishi sahihi

Kutafuta na kufanya kazi na waraghbishi sahihi kinaweza kuwa kitu cha kwanza kitakachotofautisha kampeni ya waraghbishi yenye mafanikio na ambayo imekosa mafanikio. Njia rahisi ambayo hutumika kuwapata influencers ni kwa kuwafuatilia wao pamoja na wafuasi wao.

Influencers wazuri zaidi huwa ni wale ambao wamejikita katika maeneo Fulani ambayo wao huyapenda zaidi, hivyo kuwafanya hata wafuasi wao kuwa wamewafuata kwasababu hizo. Kuna waraghbishi ambao wao huchapisha zaidi kuhusu masuala ya mitindo, afya, mazoezi, unywaji pombe, malezi, siasa, uchumi, kusafiri na kadhalika. Ni muhimu kutafuta watu wanaoendana na malengo na biashara yako na wale wenye maslahi katika sekta yako, kwani kwa kutofanya hivyo utakuwa haushawishi hadhira bali unatangaza tu. Na kuliko utumie rasilimali kutangaza kupitia waraghbishi, ni ni kheri ukawekeza katika njia nyingine za kimasoko.

Kwanini? Kwasababu lengo la waraghbishi ni kushawishi, si kutangaza. Wateja wengi wamechoka matangazo, na hutumia kila mbinu kuyakwepa, hivyo ni lazima makampuni na taasisi kutafuta njia za kuwafikia bila kuwakera.

Njia nyinginezo;

Msome mraghbishi na umtengenezee wasifu. Zingatia haya;

 • Ana wafuasi wengi wanaowasiliana nae kupitia kujibu au kusambaza kile anachoandika mtandaoni
 • Ana mahusiano mazuri na hadhira yake na aina ya wateja wako
 • Ni mtu halisi
 • Yupo mtandaoni mara kwa mara na anaweka maudhui mara nyingi
 • Ana haiba nzuri na mahusiano mazuri kwa umma
 • Kwa kuwatafuta, kuwalea, kuwafunza na kuwakuza waraghbishi ambao watakuwa mabalozi wa bidhaa na huduma zako huko mbeleni.

Ingawa, kamwe usichanganye idadi ya wafuasi na ushawishi. Mafanikio huja ikiwa kampuni zitachagua waraghbishi ambao wana ushawishi wa kweli kwa wateja na hadhira lengwa, sit u kuwa na idadi kubwa ya wafuasi mitandaoni. Utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuwa kuwa watu wenye wafuasi wachache mtandaoni wana ushawishi na mahusiano mazuri zaidi na wafuasi wao kuliko wale wenye mamilioni ya wafuasi.

3.Waamini waraghbishi katika kutengeneza maudhui

Kampuni inaweza kuwa iliwekeza katika utafiti na matumizi ya zana mbalimbali za kufahamu na kupima ni nini wateja na hadhira inataka kusikia, lakini ikiwa itafanya kazi na waraghbishi wenyewe, inaweza kutengeneza maudhui ya kimasoko au ya kimawasiliano yenya maana na matokeo zaidi.

Waraghbishi hufahamu zaidi aina ya maudhui ambayo hadhira zao zinapenda kusikia, lugha, wakati na namna bora ya kuwasilisha ujumbe mahususi. Kwa kushirikiana nao kutengeneza maudhui, nafasi ya kufanikiwa katika mpango wako ni kubwa zaidi. Kitu cha msingi cha kufanya ni kuandaa muongozo wa aina ya maudhui na matarajio yenu kama taasisi, na vilevile kuwa tayari kupitia maudhui husika kabla hayajawekwa mtandaoni.

4.Tekeleza mpango wako kwa ufanisi

Baada ya kufuata hatua zote hizo ikiwamo kutengeneza maudhui yako, kinachofuata ni kutekeleza mpango uliokuwa umeuandaa. Unapaswa kuwa unawasiliana mara kwa mara na waraghbishi wako wakati wa ufanyaji kampeni. Pia, ni vizuri ukawa unapatikana kujibu masuala, maswali na maoni ya wateja na hadhira wakati wa kampeni yako. Vilevile, unapaswa kufuatilia kwa makini kiwango cha ushiriki wa hadhira, ikiwamo likes, shares na comments.

Vilevile, uwe tayari kufanya mabadiliko yoyote pale panapokuwa na uhitaji wa kufanya hivyo. Fuatilia ikiwa mraghbishi hakuletei matokeo ambayo unakusudia, ukigundua hivyo, unaweza kuchagua kutomtumia tena katika kampeni zijazo.

5.Watunuku/Watuze Waraghbishi wako.

Usitarajie waraghbishi watafanya kazi na kampuni yako tu kwakuwa unawalipa, unapaswa kwenda mbali zaidi na kuwajali. Ikiwa kuna waraghbishi wamefanya vizuri zaidi katika kusaidia juhudi zako za kimasoko na mawasiliano ya kimkakati, usisite kuwatunuku na zaidi ya vile walivyotarajia.

Mathalani, ikiwa ni kampuni la bidhaa au huduma, badala tu ya kuwalipa fedha ili wawe mabalozi wako, unaweza kwenda mbali zaidi na kuwazawaidia huduma au bidhaa zako ambazo zinaendana nao zaidi. Vilevile, unaweza kuandaa chakula cha jioni na kuwaalika ili kuzungumza zaidi kuhusu kazi zao na namna wamesaidia kufikisha ujumbe wa biashara yako.

Kwa kufanya hivyo, unaweza kutengeneza ukaribu nao na wakahusudu zaidi biashara yako na hivyo ukafanikiwa kujenga nao mahusiano endelevu na yenye afya

6.Pima matokeo

Baada kumaliza kutekeleza kampeni yako, ni wakati wa kupima ufanisi na matokeo yake. Unapaswa kuangalia ikiwa matokeo yamefikia malengo uliyojiwekea hapo mwanzoni wakati ulipofikiria kufanya kampeni. Vilevile, unapaswa kuona ikiwa kampeni yako imeleta matokeo chanya.

Ili kufanikisha jambo hili, ni lazima ukusanye taarifa na kufananisha na kipimo chako cha mafanikio. Unapaswa kuandaa taarifa itakayoonesha utendaji kazi wa kampeni yenu, na kuangalia ikiwa imefikia viwango mlivyokusudia ukilinganisha na kiwango cha uwekezaji.

Unaweza kutumia zana mbalimbali (analytics tools) ili kuangalia jinsi ujumbe wako ulivyowafikia watu na namna walivyoupokea.

Hitimisho

Kumbuka kwamba, katika baadhi ya kampeni, matokeo huwa hayaonekani haraka au kwa kampeni za muda mfupi. Mathalani, kama ni kampeni inayokusudia kuongeza mauzo, inawezekana ukajipa muda zaidi kupima ongezeko la mauzo kulinganisha na uwekezaji wako katika kutafuta masoko.

Vilevile, hatua hizo hapo juu zitakuongoza kutengeneza programu ya waraghbishi yenye ufanisi, na kama unavyoona, yote hayo huanza na wewe kutambua malengo yako ha haimaliziki tu kwa kumalizia kampeni. Lazima upime matokeo na kuona ni kitu gani kinafanya kazi na kitu gani hakifanyi.

Je, una maoni yoyote kuhusu Makala hii ya Matumizi za Waraghbishi katika kutafuta masoko au ungependa kupata ushauri kutoka kwetu ya namna gani bora ya kufanikisha program za waraghbishi kwa biashara yako? Hata ikiwa tu unakusudia kutusalimia, tuandikie hello@serengetibytes.com na tutafurahi kusikia kutoka kwako.