Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Symantec unaonesha kwamba makampuni makubwa yanapoteza wastani wa dola milioni 4.3 au shilingi bilioni 10 za kitanzania kila mwaka duniani, hii ikitokana na makosa mbalimbali ya kimtandao. Hata kwa wataalamu wakubwa zaidi katika sekta ya mitandao ya kijamii na digitali bado kuna changamoto fulani fulani wanaweza kupitia.

Kuna makosa ya kimtandao ambayo wengi wamepitia, na pengine pamoja na utaalamu wao wanaweza wakaendelea kupitia kwa namna fulani fulani. Habari njema ni kuwa baadhi ya changamoto za mitandao ya kijamii kwa taasisi na watu binafsi zinaweza kutatulika kwa kuongeza juhudi, maarifa na kuwekeza muda zaidi katika utendaji

Yafuatayo ni mambo matano ambayo timu ya Serengeti Bytes inaamini kuwa ikiwa taasisi/kampuni/biashara zitazingatia basi wanaweza kuongeza ufanisi wao katika mitandao ya kijamii na kufikia malengo yao;

  1. Kuwa na mkakati na sera ya mawasiliano mtandaoni

Mara nyingi biashara na taasisi nyingi huingia mitandaoni kwasababu tu zimesikia ni njia mpya ya mawasiliano, mahusiano na kutafuta masoko bila kujiandaa kwa kuwa na mpango mkakati wa kidigitali (Digital Strategy) na sera ya mtandaoni (Digital Policy). Ni muhimu kuzingatia umuhimu wa kuwa na mkakati huu ambao huelezea vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na malengo na jinsi ya kuyafikia, kutambua hadhara yako, kutambua idhaa au majukwaa utakayotumia, kutambua aina ya toni ya biashara yako na aina ya maudhui utakayoweka na namna utakayoweza kufanya ufuatiliaji na tathmini na uwekezaji wako ili kuweza kupima matokeo. Ni muhimu kuwa na nyaraka hizi zitakazoongoza biashara yako, kwani hata mwajiriwa katika kitengo akiondoka, basi anayefuata atafuata miongozo iliyopo.

  1. Shiriki mijadala na kujibu maswali ya wafuasi wako kwa wakati

Ni muhimu biashara au taasisi yako ikashiriki zaidi katika mijadala inayoanzisha au mijadala ya kisekta, yaani ile ambayo huanzishwa na biashara au taasisi nyingine au hata hadhira katika sekta inayokuhusu. Katika makosa yanayofanywa na baadhi ya biashara, ni kuweka maudhui na kuyaacha bila kuwekeza muda katika kufanya mazungumzo na kupiga soga na watu wake. Biashara zinazofanikiwa zaidi na kuwa na ushiriki mzuri wa hadhira yake, ni zile zinazowekeza zaidi katika kuzungumza na hadhira yake. Kufanikisha hili, biashara nyingi kubwa na ndogo zimeajiri watu wa ndani au kampuni za nje kama Serengeti Bytes ili kusimamia kurasa zao za mitandaoni huku zenyewe zikijikita katika maeneo mengine ya biashara zao.

  1. Fanya matangazo kwa kiasi

Katika dunia ambayo kila mtu ana uwezo wa kupata taarifa zote za bidhaa au huduma kiganjani mwake, matangazo huwa si yenye ufanisi sana katika kushawishi manunuzi. Watu wengi mtandaoni hutafuta kila namna ili kuzuia wasikutane na matangazo na wakati mwingine hufikia hatua ya kutumia boti maalumu kuzuia matangazo. Ili uendelee kufanya biashara au mawasiliano yako bila kuwabughudhi hadhira yako, hakikisha unafanya matangazo ya kiasi na ya kimkakati. Mfano, zungumzia zaidi kuhusu faida kuliko sini za bidhaa zako, onesha zinavyoweza kugusa maisha ya watu badala ya ubora wake. Kwa kufanya hivyo, tena kwa kiwango cha wastani itasaidia kuendelea kukubalina na kusikilizwa na hadhira yako.

  1. Hakikisha maudhui unayosambaza katika kurasa zako yanaendana na sekta yako (retweet, repost na share)

Kama ni biashara au taasisi, shirikisha na shiriki mijadala inayohusu biashara au sekta yako pekee isipokuwa kwasababu maalumu pekee. Mfano, usisambaze jumbe au maudhui kutoka katika akaunti binafsi kwasababu tu wewe ni mmiliki ikiwa maudhui hayo hayahusiani na biashara au sekta yako. Mara nyingi, hasa kwa biashara zinazoanza na za kati, wanaosimamia kurasa za biashara hushindwa kuziacha kuwa za biashara na kuchanganya na mambo yao binafsi. Ni muhimu biashara au taasisi yako ikahakikisha kuwa inashiriki na kusambaza taarifa zinazohusu sekta au biashara yake, jambo hili linaturudisha kwenye suala namba moja, umuhimu wa kuwa na mkakati wa kidigitali.

  1. Fahamu jinsi ya kutofautisha mbinu za uendeshaji wa ukurasa binafsi na wa biashara au taasisi na epuka kuwa rasmi sana.

Kurasa binafsi na kurasa za taasisi au biashara zina mbinu tofauti katika uendeshaji na usimamizi. Lugha, toni, uchaguzi wa maneno na jinsi ya ushiriki na usambazaji katika kurasa binafsi na zile za kitaasisi hutofautiana. Hii ni sababu kubwa taasisi na biashara hupaswa kuwa na miongozo na mikakati ya matumizi ya sehemu za kidigitali kama mitandao ya kijamii.

Toni, ni moja kati ya jambo muhimu zaidi katika uendeshaji wa kurasa za kitaasisi. Tofauti na akaunti binafsi inayoweza kusema jambo lolote na karibu kwa namna yoyote ile, taasisi ina namna zake. Kutokana na mabadiliko ta tafiti za hivi karibuni, taasisi zinashauriwa kuacha kutumia lugha na toni iliyo rasmi sana, na kuanza kutumia ile ambayo inakaribisha mazungumzo na kuanzisha mjadala chanya. Nchini kwetu Tanzania, bado taasisi nyingi zimejikita katika matumizi ya lugha rasmi na isiyovutia hadhira kushiriki katika mijadala. Kwa kubadilisha lugha na toni na kuwa yenye utani kidogo, uchangamfu na kuvutia mazungumzo husaidia kuongeza kiwango cha ushiriki wa hadhira yako.

Hayo ni mambo matano ambayo kwa siku ya leo tumeona tukushirikishe kuhusu mitandao ya kijamii.

Je una swali au maoni yoyote, au ungependa kupata ushauri wa namna ya kutumia mitandao yako ya kijamii kwa ufanisi Zaidi? Tuandikie baruapepe leo, hello@serengetibytes.com